Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuzisaidie jamii zinazoondokana na ukeketaji katika jitihada zao- Ban

Tuzisaidie jamii zinazoondokana na ukeketaji katika jitihada zao- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametoa wito zisaidiwe jamii ambako ukeketaji wa wanawake unafanyika, wakati zinapofanya jitihada za kuondokana na tabia hiyo yenye madhara kwa wanawake.

Ban amesema hayo wakati wa hafla maalum ya kuzindua ishara ya kuchagiza nguvu za kutimiza malengo ya dunia kupitia kutokomezwa kwa ukeketaji ifikapo mwaka 2030, akisema hafla hiyo inasherehekea uwezaji wa wanawake.

“Leo nina furaha kuzindua ishara hii ya kimataifa yenye nguvu. Inakumbusha kila mtu kuhusu mamilioni ya wasichana na wanawake waliokeketwa, na ni ishara ya wito wa kuchukua hatua ili kutokomeza tabia hii yenye madhara. Hili litakuwa bango letu katika safari ya kwenda mbele, tunapoonyesha dhamira yetu ya kutokomeza ukeketaji ifikapo mwaka 2030.”

Katibu Mkuu amesema, tangu mwaka 2007, zaidi ya nnchi kumi zimepitisha sheria za kukabiliana na ukeketaji, na kwamba karibu nchi zote kunakofanyika ukeketaji zimepiga marufuku kitendo hicho, akipongeza jamii zinazoathiriwa kwa juhudi zao.

Nimehamasishwa hasa na jamii zinazotafuta njia mbadala za kuwaweka wasichana jandoni. Maelfu ya wasichana wamenufaika kutokana na njia hizi mbadala. Nchini Kenya na Tanzania, badala ya kukeketwa, wasichana hukaa wiki moja mbali na familia zao ili kujifunza stadi za maisha. Palipokuwa na mateso, sasa pana nguvu.”

Ban ametoa wito iendelezwe kampeni ya kuwawezesha wasichana hao na wengine wengi, na kujikita zaidi katika elimu badala ya ukeketaji.