Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi za Amerika zishirikiane na UM kutatua matatizo ya dunia: Ban

Nchi za Amerika zishirikiane na UM kutatua matatizo ya dunia: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye yuko mjini Washington D.C kwa shughuli mbali mbali, siku ya Jumatano ametoa wito kwa nchi za Amerika kushirikiana na Umoja huo katika kutatua matatizo yanayokabili dunia hivi sasa.

Bwana Ban katika hotuba yake kwa Baraza la Kudumu la Ushirikiano wa nchi za Amerika, OAS, amesema bara la hilo limeendelea kuwa na ushawishi mkubwa duniani hasa wakati huu ambapo uchumi wa nchi zilizo kwenye ukanda huo unakua na taasisi za kidemokrasia zinaimarika.

Amesema ushirikiano wenye manufaa ya kudumu na endelevu kati ya Umoja wa Mataifa na chombo hicho ni muhimu kwa kuwa anashawishika ya kwamba Umoja huo una dhima kubwa kwenye eneo hilo kama ilivyo dhima ya bara la Amerika ndani ya Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema nchi hizo zina uzoefu, fikra na mawazo ambayo yanaweza kuchagiza upatikanaji wa suluhisho la mambo mbali mbali duniani.