Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OECD na UNHCR watoa wito wa kuongeza sera za kuwajumuisha wakimbizi:

OECD na UNHCR watoa wito wa kuongeza sera za kuwajumuisha wakimbizi:

Mkuu wa Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) Ulaya na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi(UNHCR),kwa pamoja wametoa wito kwa serikali kuongeza juhudi za kusaidia wakimbizi kujumuishwa katika jamii na kuchangia katika jamii na uchumi barani Ulaya.

Wakizungumza kwenye mkutano wa ngazi ya juu wa masuala ya ulinzi na ujumuishi wa wakimbizi mjini Paris wamesema mwaka 2015 watu zaidi ya milioni moja wameingia Ulaya kutafuta hifadhi huku wengine milioni 1.5 wakiomba ukimbizi katika mataifa ya OEDC.

Mashirika hayo mawili yamesisitiza kwamba sio tu ni wajibu kuwasaidia bali pia faida za kiuchumi za kuwasaidia mamilioni ya wakimbizi kupata ujuzi wanaohitaji ili kufanya kazi ipasavyo na kwa usalama ni muhimu sana.

Wameongeza kuwa ili wakimbizi waweze kuwajibika kijamii, kiuchumi na kitamaduni katika nchi wanakopata hifadhi wanahitaji haki sawa na fursa na sera muafaka zitafanikisha hilo.