Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kobler alaani vikali utekaji wa mbunge Libya, ataka aachiliwe mara moja

Kobler alaani vikali utekaji wa mbunge Libya, ataka aachiliwe mara moja

Mwakilishi wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, UNSMIL, Martin Kobler, amelaani vikali utekaji wa mbunge Mohamed al-Ra’id, na kutaka mbunge huyo aachiwe huru mara moja bila masharti yoyote.

Bwana al-Ra’id alitekwa nyara hapo jana akiwa njiani kuelekea uwanja wa ndege, baada ya kushiriki kikao cha wawakilishi wa bunge huko Tobruk.

Kobler ameeleza kukerwa na kitendo hicho, na kutoa wito kwa wote wenye ushawishi wafanye kila wawezalo ili kuhakikisha mbunge huyo anaachiliwa.

Ameongeza kuwa mbunge huyo asiadhibiwe kwa uamuzi wake jasiri wa kuendelea kujali maslahi ya nchi na kuweka maisha yake hatarini kwa kujiunga na bunge, kulingana na makubaliano ya kisiasa ya Libya.