Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjini Abu Dhabi Ban Ki-moon atoa wito kwa uchumi unaojali mazingira

Mjini Abu Dhabi Ban Ki-moon atoa wito kwa uchumi unaojali mazingira

Leo mijini Abu Dhabi, kwenye Falme za Kiarabu, UAE, kumezinduliwa kongomano kuhusu nishati za baadaye, ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema nishati endelevu kwa bei nafuu zitachangia pakubwa katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuokoa maisha ya watu milioni 4.3 wanaofariki kila mwaka kutokana na vyanzo duni vya nishati, akieleza matumaini yaliyopo sasa:

(Sauti ya Ban)

“Kupungua kwa bei ya nishati mbadala, hasa nishati ya jua, kumezifanya nishati endelevu kuwa na bei nafuu na kuweza kuwafikia watu maskini zaidi duniani. Kizazi kipya cha vyombo vinavyotumia nishati kwa ufanisi zaidi kimewapatia watu fursa ya huduma za umeme, joto, mawasiliano na vifaa vingine wanavyohitaji.”

Wakati huo huo bwana Ban amezindua Siku ya kuchukua hatua ya Abu Dhabi akizisihi serikali na sekta binafsi kuendelea kuwekeza katika miradi rafiki kwa mazingira.