Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO imefungua kituo kipya cha dharura na polio Jordan

WHO imefungua kituo kipya cha dharura na polio Jordan

Kama sehemu ya kuimarisha shughuli zake za dharura kanda ya Mashariki ya Kati na kupambana na polio Shirika la Afya Duniani (WHO) limefungua kituo cha kikanda kwa ajili ya dharura za kiafya na kutokomeza polio mjini Amman, Jordan.

Kwa mujibi wa WHO idadi ya watu wanaohitaji huduma za kiafya za dharura ni kubwa sana kutokana na madhila mengi na hali huo inatoa shinikizo kubwa kwa shirika la afya duniani wakati huu kuliko wakati mwingine wowote.

Theluthi mbili ya nchi za Mashariki ya Kati zinakabiliwa na vita au kuathirika na vita huku zaidi ya nusu ya wakimbizi wote duniani wanatoka katika ukanda huo, na pia ndio ukanda wenye wakimbizi wa ndani wengi zaidi kuliko kwingine kokote duniani amesema Dr Ala Alwan mkurugenzi wa kanda wa WHO.

Amezitaja nchi za Iraq, Syria na Yemen kuwa ni miongoni mwa nchi za ukanda huo zinazohitaji muendelezo wa msaada wa kibinadamu wa afya. Amesema mbali ya mahitaji ya dharura ya kibinadamu ukanda mzima pia unaendelea kukabiliana na hatua ya mwisho ya kutokomeza polio ambayo baraza la afya duniani limetangaza kuwa ni tatizo la dharura la kiafya linalotia hofu kimataifa.

WHO imesema mwaka 2015 umekuwa wa mafanikio katika kufikia lengo la kutomomeza polio.