Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yapambana na kipindupindu kwenye kambi ya Dadaab Kenya:

UNHCR yapambana na kipindupindu kwenye kambi ya Dadaab Kenya:

Wahudumu wa afya kwenye kambi kubwa kabisa ya wakimbizi duniani ya Dadaab Kenya, wanajitahidi kupambana na mlipuko wa kipindupindu ambao tayari umeshakatili maisha ya watu 10 na wengine takriban 1000 wameambukizwa tangu ulipozuka mwezi uliopita ukihusishwa na mvua kubwa za El Niño.

Kipindupindu ugonjwa hatari unaouwa kutokana na bakteria,na husababisha homa kali, kutapika na kuhara uliingia Dadaab katikati ya mwezi Novemba kwenye kambi hiyo inayohifadhi wakimbizi na waomba hifadhi 347,000 wengi wao ni wanaokimbia machafuko nchini Somalia.

Jopo maalumu la kukabilina na mlipuko huo linalojumuisha wafanyakazi wa UNHCR na mashirika wadau, limekuwa likifanya kazi kutwa kucha kwa ushirikiano na wizara ya afya ya Kenya na kitengo cha masuala ya wakimbizi kutibu walioathirika na kuzuia kuenea zaidi kwenye kambi hiyo iliyoko Kaskazini Mashariki mwa Kenya.

Kwa mujibu wa UNHCR vituo vinne vimezinduliwa katika kambi hiyo kutibu na kupambana na kipindupindu. Kila kituo kinaweza kutibu wagonjwa 50 na kugawa dawa. Kambi ya kwanza ya Hagadera Daadab ilianzishwa mwaka 1991 wakati watu walipokuwa wakikimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Somalia na kuingia Kenya.