Hali ya njaa yazidi kuwa mbaya Taiz Yemen: WFP
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula WFP limeelezea leo wasiwasi wake kuhusu kuzorota kwa hali ya kibinadamu mjini Taiz nchini Yemen ambapo watu hukumbwa na njaa huku WFP ikishindwa kuwapelekea chakula.
Kwenye taarifa iliyotolewa leo, Mkurugenzi wa kikanda wa WFP Muhannad Hadi amenukuliwa akisema mapigano mjini Taiz yameizuia WFP kufikia watu wanaohitaji, akitoa wito kwa pande zote za mzozo kuruhusu msaada wa chakula kuingia mjini humo.
Kwa ujumla, WFP imefanikiwa kupeleka tani 6,600 za vyakula vikiwemo unga wa ngano, kunde, mafuta na sukari kwenye maghala mbalimbali ya jimbo la Taiz kwa kipindi cha miezi michache iliyopita.
WFP imeongeza kwamba Taiz ni moja ya majimbo 22 ambapo hali ya ukosefu wa chakula ni mbaya zaidi.
Kwa mujibu wa WFP, watu milioni 7.6 nchini Yemen hawana uhakika wa chakula na wanahitaji msaada wa dharura ili kuokoa maisha yao.