Skip to main content

COP 21 ilete mabadiliko ya dhati: Ban Ki-moon

COP 21 ilete mabadiliko ya dhati: Ban Ki-moon

Mkutano wa 21 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadilikoya tabianchi umeanza leo huko Paris, Ufaransa ukifunguliwa rasmi na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon. John Kibego na taarifa kamili.

(Taarifa ya Kibego)

Katika hotuba yake ya uzinduzi, Ban amewasihi viongozi zaidi ya 150 wanaohudhuria mkutano huo kuafikiana kuhusu mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, akitaka mkutano huo uweke hatua ya kihistoria.

Amekaribisha michango iliyotangazwa tayari na nchi 180 kuhusu juhudi zao za kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi, akisema ni mwanzo mzuri, lakini bado juhudi kubwa zaidi zinahitajika ili kudhibiti ongezeko la halijoto duniani chini ya nyuzi 2 za Selisiasi, akikumbusha kwamba ongezeko hilo tayari litakuwa na matokeo makubwa kwa upatikanaji wa chakula na maji duniani.

Amerejelea mapendekezo manne anayosema kuwa ni msingi wa COP21 ambayo ni mkataba uwe endelevu, uende na wakati, uonyeshe mshikamano na ukubalike na pande zote na zaidi hayo amegusia suala ambalo limekuwa linaleta mvutano....

(Sauti ya Ban)

“Mkataba mpya lazima ujumuishe mfumo mmoja ulio wazi wa kupima matokeo, kufuatilia na kuripoti maendeleo. Na nchi ambazo zinatoa kiwango kidogo cha gesi chafuzi zipatiwe usaidizi ili ziweze kukidhi mahitaji ya mfumo mpya utakaokubaliwa.”