Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uharamia Somalia, Baraza la usalama lapitisha azimio

Uharamia Somalia, Baraza la usalama lapitisha azimio

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio ambalo pamoja na mambo mengine limesema vitendo vya uharamia na uporaji kwenye pwani ya Somalia vinazidi kutishia amani na usalama nchini humo na ukanda mzima kwa ujumla.

Azimio hilo lililopitishwa leo kwa mantiki hiyo linatambua hatua zinazochukuliwa na Somalia yenyewe pamoja na Kenya, Mauritius, Seychelles na Tanzania katika kuwafungulia mashtaka watuhumiwa wa vitendo vya uharamia kwenye eneo hilo.

Halikadhalika linasisitiza kuwa vikwazo vya silaha dhidi ya Somalia kwa mujibu wa maazimio ya awali hayalengi shehena za silaha zinazotumiwa na Somalia yenyewe nan chi wanachama wa Umoja wa Mataifa katika kupambana na uharamia.

Pamoja na kulaani vitendo vya uharamia, wajumbe wa Baraza la Usalama wametambua juhudi zinazoendelea za kudhibiti ambazo zimewezesha kupungua kwa matukio ya uharamia na hivyo kuomba nchi wanachama kuendeleza ushirikiano wao na Somalia kukabili vitendo hivyo.