Skip to main content

Tahadhari yatolewa kuhusu uhalifu dhidi ubinadamu Burundi, serikali yajibu

Tahadhari yatolewa kuhusu uhalifu dhidi ubinadamu Burundi, serikali yajibu

Viongozi wa Burundi wameonywa dhidi ya kueneza chuki, na kuchochea ghasia zinazoweza kuzua mauaji ya halaiki. Taarifa kamili na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Onyo hiyo imetolewa Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari, Adama Dieng, akilihutubia Baraza la Usalama Jumatatu jioni, baada ya onyo kama hiyo kutolewa na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Zeid Ra’ad Al Hussein.

Akitaja mfano wa hotuba ya Rais wa Seneti ya Burundi aliyosema ilikuwa na maneno ya kuchochea na vitisho, Bwana Dieng amesema matamshi yake yalifanana sana na yale yaliyotumiwa kabla ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994.

“Kwa hiyo ni muhimu kwa rais na viongozi wa ngazi ya juu kujiepusha na kutoa matamshi yoyote yanayoweza kudhaniwa kuwa yanawachochea watu kutenda uhalifu dhidi ya raia wenzao. Kufanya hivyo ni hatari na kutowajibika, na kumepingwa chini ya sheria ya kimataifa”.

Akiongea kwa njia ya video kutoka Bujumbura, Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, Alain Aimé Nyamitwe amesema kwamba serikali ya Burundi inaendelea kushiriki kwenye mchakato wa mazungumzo.

" Licha ya taarifa zinazosambazwa na upinzani wenye itikadi kali na baadhi ya vyombo vya habari, Burundi haiteketei. Visa vichache vya uhalifu vyenye lengo la kuvutia nadhari ya jamii ya kimataifa vinakaribia kudhibitiwa. Jinsi unavyojua, usalama ndio msingi. Bila usalama hakuna kitendo kizuri wala maendeleo ambayo yanawezekana."