Skip to main content

WFP yarejesha usambazaji chakula CAR

WFP yarejesha usambazaji chakula CAR

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limeanza tena kupeleka msaada wa chakula nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, baada ya kulazimika kusitisha kutokana na ghasia za hivi karibuni.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric amesema tayari wiki hii pekee, WFP imefikishia misaada ya chakula watu zaidi ya Elfu Thelathini kwenye mji mkuu Bangui, idadi ambayo ni wakimbizi wapya wa ndani.

Amesema watu hao wamekuwepo bila msaada wa chakula kwa siku kadhaa na wameenea katika vituo zaidi ya 20.

Kwa mujibu wa WFP mtu mmoja kati ya Wanne mjini humo anahitaji msaada wa chakula.

Wakati huo huo, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini CAR, MINUSCA umesema jitihada zinaendelea kuandikisha wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.

Hadi Jumanne, asilimia 87 ya wananchi walishaandikishwa na kwamba jitihada za sasa ni kufikia wakimbizi walio nchi jirani ili uchaguzi huo uwe jumuishi.