Skip to main content

Uzalishaji wa Afyuni wapungua Afghanistan: UNDOC

Uzalishaji wa Afyuni wapungua Afghanistan: UNDOC

Kwa mujibu wa takwimu mpya za utafiti wa hivi karibuni wa pamoja kati ya Wizara ya kukabiliana na mihadarati nchini Afghanistan na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Madawa ya Kulevya na Uhalifu, UNODC, uzalishaji wa zao la Afyuni nchini humo umepungua kwa asilimia 19 mwaka huu, ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Taarifa ya pamoja ya pande mbili hizo imesema kupungua huko kumezingatiwa kutokana na kupungua kwa eneo la kilimo hicho ambapo mwaka huu ni takribani ekari 183,000 , ikilinganishwa na ekari 224,000 mwaka 2014.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNODC, Yury Fedotov, amekaribisha habari hizo akisema ni njema na kwamba anatumaini utafiti huo utatumiwa katika kutengeneza sera thabiti za kuendeleza juhudi hizo muhimu.

Aidha Fedetov amesema kuendeleza juhudi hizo inategemea uamuzi wa serikali ya Afghanistan na jumuiya ya kimataifa , ambayo ni lazima ijishughulishe ipasavyo katika kutoa raslimali zinazohitajika na kutoa ahadi ya muda mrefu ya kushughulikia tishio la mihadarati kwa jamii.