Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlipuko wa kipindupindu waripotiwa Uvira, DR Congo

Mlipuko wa kipindupindu waripotiwa Uvira, DR Congo

Jimbo la Kivu Kusini huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC limetangaza mlipuko wa kipindupindu kwenye mji wa Uvira.

Maafisa wa afya wanasema hadi sasa watu 180 wameugua ugonjwa huo huku wawili wakifariki dunia katika kipindi cha wiki mbili sasa katika mji huo ambao kila mwezi inasajili wagonjwa 660 wa kipindupindu.

Taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya ofisi ya usaidizi wa kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, OCHA inasema licha ya wataalamu wa afya na wadau wa kibinadamu kukutana tarehe 29 mwezi uliopita na kusema wanaweza kukabili ugonjwa huo, changamoto inayosalia ni kupata suluhu la kudumu dhidi ya ugonjwa huo unaoripotiwa kuota mizizi kwenye jimbo hilo.

Tayari mlipuko mwingine wa kipindupindu umeripotiwa kwenye jimbo la Maniema nchini DRC.