Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamati ya UM yapongeza Somalia kwa kuridhia mkataba wa haki ya mtoto

Kamati ya UM yapongeza Somalia kwa kuridhia mkataba wa haki ya mtoto

Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Mtoto, imekaribisha hatua ya Somalia kuridhia Mkataba kuhusu Haki za Mtoto mnamo Oktoba mosi 2015, na kutoa wito nchi zote duniani ziuridhie mkataba huo.

Akiipongeza Somalia kama nchi ya 196 kufanya kuridhia mkataba huo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Benyam Dawit Mezmur, amesema kuuridhia mkataba huo ni hatua muhimu inayoenda sambamba na ahadi ya kuutekeleza.

Mkataba huo, ambao ndio mkataba wa kimataifa wa haki za binadamu ulioridhiwa kwa wingi zaidi, unazingatia baadhi ya haki za watoto, zikiwemo haki ya kuishi, kuwa na afya, kupata elimu na kucheza, kuwa na familia, kulindwa dhidi ya ukatili, kutobaguliwa na maoni yao kusikilizwa.

Kamati hiyo imesema inatazamia kuridhiwa kwa mkataba huo na Marekani, ikiwa ndiyo nchi pekee iliyosalia kuuridhia mkataba huo, na kutoa wito kwa nchi wanachama ziridhie vipengele vitatu vya sheria ndani yake vinavyohusika na masuala ya kuuza watoto, kutumikisha watoto katika biashara ya ngono na katika picha na video za ngono.