Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu akaribisha mapendekezo ya nchi 147 za hatua kuhusu tabianchi

Katibu Mkuu akaribisha mapendekezo ya nchi 147 za hatua kuhusu tabianchi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekaribisha mapendekezo ya mipango ya kitaifa kuhusu tabianchi kutoka kwa nchi 147, ambazo huchangia asilimia 85 ya uzalishaji wa hewa chafuzi duniani.

Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wake, Ban amesema kuwasilishwa kwa mapendekezo hayo mnamo Oktoba mosi kunatoa msingi imara wa kufikia mkataba wa dunia nzima kuhusu tabianchi mjini Paris, Ufaransa, mwezi Disemba.

Akiitaja kama hatua nzuri na kuzhimiza nchi zilizosalia kuwasilisha mapendekezo yao, Katibu Mkuu ametoa wito kwa nchi wanachama zijumuishe vipengele katika mkataba wa Paris vitakavyoziwezesha kuufanyia marekebisho mara kwa mara na kuimarisha viwango vya ari na utashi wa ahadi zao za kitaifa kulingana na sayansi.

Amesema mkataba huo wa Paris unapaswa kuwa hatua ya mapinduzi, na utume ujumbe mzito kwa wananchi na sekta binafsi kuwa mabadiliko ya uchumi wa kimataifa ni sharti yawepo, ni ya manufaa, na tayari yameanza.