Obama ataja mambo ya kuzingatia kuimarisha ulinzi wa amani
Marekani leo imeongoza mkutano wa viongozi kuhusu ulinzi wa amani kwenye Umoja wa Mataifa ambapo Rais Barack Obama ametaja mambo manne ya kuzingatia katika kuimarisha mpango huo.
Mosi ametaka nchi kuchangia zaidi askari na pili kuimarisha ulinzi wa raia akisema tofauti na miaka 20 iliyopita, walinda amani sasa wana mamlaka za kuchukua hatua zaidi kulinda raia lakini hilo lifanyike kote kwani kuna maeneo wanakumbwa na mashambulizi.
Hata hivyo akasema lazima kuepusha udhalilishaji unaofanywa na walinda amani dhidi ya raia akisema..
(Sauti ya Rais Obama)
"Nataka nieleweke! Kuna idadi kubwa ya walinda amani wanafanya shughuli zao kwa heshima kubwa sana. Lakini tumeshuhudia visa vingi vya kusikitisha vya walinda amani wakidhalilisha raia, ikiwemo kuwabaka, na udhalilishaji wa kingono. Hii haikubaliki kabisa. Katibu Mkuu naunga mkono unavyoshughulikia suala hili na na kama viongozi na jamii ya kimataifa lazima tusisitize kutokuvumilia kabisa udhalilishaji huu.”
Suala la tatu alililosisitiza ni kuboresha operesheni za ulinzi wa amani ziwe za kisasa zaidi na nne ni kuimarisha juhudi za kidiplomasia kuzuia mizozo isitokee.