Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asilimia 90 ya wazee Afrika wanakosa huduma: ILO

Asilimia 90 ya wazee Afrika wanakosa huduma: ILO

Kuelekea siku ya wazee duniani tarehe Mosi mwezi ujao, shirika la kazi duniani, ILO limesema kuna uhaba wa watoa huduma Milioni 13 nukta sita ulimwenguni kote na hivyo kudumaza huduma za uangalizi kwa zaidi ya nusu ya wazee duniani.

ILO katika utafiti wake mpya imebaini kuwa uhaba huo unakosesha huduma za muda mrefu za malezi kwa watu Milioni 300 wenye umri wa miaka 65 na zaidi duniani.

Mathalani ripoti hiyo inasema Afrika ina uhaba wa wahudumu Milioni Moja na Nusu na hivyo kusababisha zaidi ya asilimia 90 ya wazee kukosa huduma.

Kwa mantiki hiyo ILO inataka fursa za ajira katika nyanja hiyo ili wazee waweze kupata huduma zao za msingi kwa muda mrefu sambamba na kuweka mifumo ya hifadhi ya jamii inayolenga wazee.