Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushiriki wa jamii kwenye maendeleo ni siri ya mafanikio nchini Rwanda: Kagame

Ushiriki wa jamii kwenye maendeleo ni siri ya mafanikio nchini Rwanda: Kagame

Uhusiano baina ya raia na viongozi wao ni msingi katika kutimiza malengo ya maendeleo, amesema leo Rais wa Rwanda Paul Kagame akihudhuria kongamano la kimataifa kuhusu maendeleo endelevu lililofanyika jumatano na alhamis hii kwenye chuo kikuu cha Columbia mjini New York, Marekani.

Kwenye hotuba yake aliyotoa mwisho wa mkutano huo uliohusisha Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson, na viongozi wengine wa Umoja wa Mataifa, Bwana Kagame amepongeza mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia au MDGs. Akichukua mfano wa Rwanda amesema nchi hiyo imejitahidi katika kutimiza MDGs kwa sababu raia walikuwa na hamu ya kuona mabadiliko kwenye maisha yao na uaminifu na viongozi wao.

Bwana Kagame amesisitiza kwamba ili maendeleo yawe endelevu, ufadhili na mikakati pekee hautoshi, bali pia ni lazima kuhakikisha kwamba raia wanashirikishwa ipasavyo na kujenga nuru ya kitaifa.

“ Tunafanya kazi ili kuwapatia raia jinsi na nyenzo za kubadilisha maisha yao, lakini ni muhimu pia kuchukua muda kuungana nao kwa sababu hatimaye ni wale wanaotekeleza ufumbuzi huo mzuri. Kwa kifupi maendeleo yanapatikana wakati ambapo raia wanaaminia lengo na kasi ya mabadiliko.”