Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna uhusiano baina ya mizozo, umaskini na uhamiaji- Graziano da Silva

Kuna uhusiano baina ya mizozo, umaskini na uhamiaji- Graziano da Silva

Mamilioni ya watu wanaolazimika kuhama makwao wakikimbia vita, umaskini na taabu nyinginezo, ni ukumbusho wa haja ya dharura ya kupata ufumbuzi wa amani kwa misingi ya haki ya kijamii na fursa bora za kiuchumi kwa wote.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo, FAO, José Graziano da Silva, ambaye pia amesema njia bora ya kupata ufumbuzi huo wa amani ni kuwekeza na kulinda uwekezaji katika maeneo ya vijijini.

Bwana da Silva amesema maendeleo na uhakika wa chakula vijijini ni sehemu muhimu ya jitihada za kimataifa za kukabiliana na mzozo wa wakimbizi. Ameongeza kuwa vita husababisha njaa, na njaa huua na kuwalazimu watu kuhama makwao.

Mkuu huyo wa FAO amesema, kuunga mkono vitega uchumi vya kilimo kunaweza kuchangia kuwasaidia watu kuishi kwenye ardhi zao wanapojihisi salama kufanya hivyo, na kuweka mazingira ya kurejea kwa wakimbizi, wahamiaji na watu walolazimika kuhama.