Rais wa UNGA70 aangazia vipaumbele na mtazamo kuhusu Syria

Rais wa UNGA70 aangazia vipaumbele na mtazamo kuhusu Syria

Ni Rais wa mkutano wa 70 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Mogens Lykketoft kutoka Denmark akitangaza kufunguliwa rasmi wa kikao cha kwanza cha mkutano huo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani siku ya Jumanne.

Tangazo hilo lilifuatiliwa na dakika moja ya wajumbe kusimama na kuwa kimya ikiwa ni fursa ya tafakuri na hatimaye Bwana Lykketoft akaanza hotuba yake iliyoangazia masuala kadhaa ikiwemo umuhimu wa mkutano huo ambao utashuhudia kuridhiwa kwa malengo ya maendeleo endelevu au ajenda 2030 ambayo amesema wakuu wa nchi wanachama wanaamua bila shinikizo kusongesha mustakhbali wa dunia kwa kizazi cha sasa na vijavyo.

Na hatimaye akataja mijadala ya ngazi ya juu ya kimaudhui itakayofanyika msimu wa chipukizi mwakani ambapo cha kwanza ni kuhusu utekelezaji wa Malengo ya maendeleo endelevu, mabadiliko ya tabianchi na uchangishaji wa fedha. Mjadala wa pili kuhusu amani na usalama na tatu kuhusu haki za binadamu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akatanabaisha..

(Sauti ya Ban)

“Mfumo wa Umoja wa mataifa umejiandaa kusaidia ufanikishaji wa malengo hayo.”

Nje ya ukumbi waandishi wa habari walipata fursa ya kumuuliza maswali ambapo mmoja alitaka kufahamu mtazamo wake kuhusu hatma ya janga la wakimbizi barani Ulaya na mzozo wa Syria ambapo Rais huyo wa Baraza Kuu amesema mzozo umedumu muda mrefu, sasa ni mwaka wa tano….

(Sauti ya Mogens)

“Ni kwa sababu nchi zenye ngumu duniani na katika kanda hawajaweza kuafikiana jinsi ya kusitisha hivi vita na janga la kibinadamu. Nadhani sote tuna matumaini katika ukumbi huu kuwa hilo litabadilika, kwamba nchi tano zenye ujumbe wa kudumu kwenye baraza la usalama na nchi zenye ushawishi kwenye ukanda huo zinaweza kuafikiana.”

Alipoulizwa kuhusu marekebisho ya baraza la usalama amesema atasongesha mbele harakati zilizoanzishwa na mtangulizi wake Sam Kutesa na kwamba misingi itakuwa ni azimio lililopitishwa na mkutano wa 69 wa baraza kuu, halikadhalika suala la uchaguzi wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa mujibu wa azimio lililopitishwa.