Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamilioni ya watoto nchini Syria wakosa elimu: UNICEF

Mamilioni ya watoto nchini Syria wakosa elimu: UNICEF

Zaidi ya watoto milioni mbili nchini Syria hawataingia shuleni mwaka huu, wakati ambapo shule zinafunguliwa upya, limesema leo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudhumia Watoto UNICEF.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo, UNICEF imesema watoto wengine 400,000 wako hatarini kuacha shule mwaka huu kutokana na ghasia na vita.

Akiongea na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi msemaji wa UNICEF Christophe Boulierac amesema watoto wengine nchini Syria hawajawahi kwenda shuleni, mzozo ukiwa unaendelea kwa zaidi ya miaka minne.

“ Shule 5,000 nchini humo haziwezi kutumiwa kwa sababu zimeharibiwa au kugeuzwa sehemu ya kuhifadhi wakimbizi wa ndani au kambi za wanajeshi. Mwaka 2014, shule 60 zilishambuliwa,na hayo yanaenaendelea mwaka huu wa 2015, ingawa hatuna takwimu za mwisho kwa sasa hivi.”

Kwa mujibu wa mwakilishi wa UNICEF nchini Syria, Hanaa Singer, watoto milioni nne wamefanikiwa kuhudhuria masomo mwaka jana, huku UNICEF na wadau wake wakisaidia karibu watoto milioni tatu waliokosa mafunzo na kuwasaidia kuwarudishia shuleni.