Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtalaam wa UN akariri tahadhari yake kuhusu Burundi

Mtalaam wa UN akariri tahadhari yake kuhusu Burundi

Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya mpito Pablo de Greiff amesema mwelekeo wa Burundi sasa ni kinyume na mafanikio yaliyopatikana tangu makubaliano ya amani ya Arusha ya mwaka 2000.

Akiwasilisha ripoti yake kuhusu ziara yake nchini humo katika Baraza la Haki za Binadamu linaloendelea mjini Geneva Uswisi, Bwana De Greiff amesema desturi ya ukwepaji sheria inayoendelea nchini humo kwa kipindi cha miongo iliyopita imewezesha ghasia iliyotokea nchini humo mwaka huu.

Amesema hatua za dharura zinapaswa kuchukuliwa ili kuzuia mauaji mengine yasitokee tena, huku suala la Burundi likiwa limekwama kwa ngazi ya Baraza la Usalama.

"Natahadharisha jamii ya kimataifa, taasisi za kimataifa na kikanda, kwamba hawawezi kuendelea kukaa na kusubiri mauaji mengine ya halaiki yatokee. Watu nchini Burundi na kwenye ukanda huo wamepitia mateso yasiyojulikana na ukiukaji mbaya zaidi."