Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yatoa mwongozo wa kinga na tiba ya Ebola dhidi ya wajawazito

WHO yatoa mwongozo wa kinga na tiba ya Ebola dhidi ya wajawazito

Shirika la afya duniani, WHO limetoa mwongozo kuhusu uchunguzi na kinga kwa mwanamke mjamzito na anapojifungua endapo kuna mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.

Mwongozo huo wa mpito unatolewa kwa wajawazito ambao wanaweza kuwa hatarini kuambukiza wengine, au wale ambao wamepona Ebola na wanaweza kuambukiza au wale walio karibu na wagonjwa wa Ebola.

Mathalani mwongozo huo ambao utapitiwa upya baada ya mwaka mmoja unataka uangalifu wa hali ya juu ikiwemo matumizi vya vifaa vya kinga kama vile sare maalum, barakoa vinatumika wakati wa kumsaidia mjamzito kujifungua ili kuhakikisha majimaji ya mwilini na damu havisababishi maambukizi.

Halikadhalika iwapo mama alikuwa karibu na wagonjwa wa Ebola, uchunguzi wa kina ufanyika haraka kwa yeye na mtoto wake kufahamu iwapo wameambukizwa virusi vya Ebola au la.

Muongozo umesema iwapo mama na mwanae watabainika kuwa na maambukizi, watengwe katika vituo vya tiba dhidi ya Ebola.

Mwongozo huo umetolewa wakati kumeripotiwa wagonjwa wapya wawili wa Ebola, mmoja huko Conakry- Guinea na mwingine Kambia nchini Sierra Leone.