Hali CAR imetengamaa, lakini bado inatia wasiwasi- Kamishna Zeid
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Zeid Ra’ad Al Hussein, ambaye yupo ziarani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, amewaambia waandishi wa habari mjini Bangui kuwa ingawa hali nchini humo imeboreka ikilinganishwa na kilele cha mgogoro mwishoni mwa mwaka 2013 na mapema 2014, bado inatia wasiwasi kwa raia wa CAR na kwa Umoja wa Mataifa.
Kamishna Zeid amesema serikali ya mpito nchini CAR inaweza kujivunia hatua kadhaa katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita, ikiwemo kuanzisha mashauriano yaliyoibua mapendekezo ya nini kifanyike na kuweka njia ya taifa hilo kufuata linapojaribu kusaka amani na usalama, pamoja na maridhiano.
Licha ya hayo, Kamishna Zeid amesema taifa hilo bado limeghubikwa na uoga, na watu wake bado wamegawanyika sana kufuatia mgogoro uliovunja mifumo ya kijamii, kitamaduni, kisiasa na kiuchumi, na kusababisha takriban watu milioni moja kuhama makwao, aghalabu kwa misingi ya kidini au kabila.
Kuhusu haki za binadamu, Kamishna Zeid amesema haki na usalama ni masuala yanayoambatana, na kwamba juhudi zaidi zahitajika ili kubadili mzunguko wa sasa wa ukatili na ukwepaji sharia.
Kuhusu madai ya unyanyasaji wa kingono uliofanywa na walinda amani, amesema kwamba hakuna kisingizio chochote kinachoweza kukubalika kwa vitendo kama hivyo.