Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC isaidiwe uchaguzi uwe huru na wa haki

DRC isaidiwe uchaguzi uwe huru na wa haki

Wakati uchaguzi mkuu ukibisha hodi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DCR), timu ya wajumbe na wawakilishi wa kimataifa katika ukanda wa Maziwa Makuu, imetoa wito kwa wadau wa kisiasa kukubaliana kuhusu masharti katika mchakato wa uchaguzi.

Baada ya mkutano wao mjini Geneva, Uswisi, wajumbe hao ambao ni pamoja na Mjumbe maalum wa Katibu Mkuuwa Umoja wa Mataifa Said Djinnit na Mjumbe Maalum wa Marekani Thomas Perriello, wamesisitiza umuhimu wa kuisaidia DRC katika uchaguzi wa kihistoria, ambao ni muhimu kwa maendeleo na usalama wa taifa hilo.

Aidha, wamebaini umuhimu wa uamuzi wa mapema wa hatua za kuhakikisha uhuru wa watu kugombea, uhuru wa vyombo vya habari na kuweka mazingira rafiki ya kusaka ufuasi kwa wagombea wote.

Wamesema kwa kuungwa mkono na jamii ya kimataifa, uchaguzi huo utakuwa wa wazi, kuaminika, na jumuishi.

Wameongezea kuwa ni vyema uchaguzi wa raisi na wabunge ufanywe katika siku zilizobainishwa katika katiba na kujumuisha watu wote wenye sifa za kuchagua.