Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban afurahia ajenda ya maendeleo endelevu

Ban afurahia ajenda ya maendeleo endelevu

“Nina habari nzuri kwa wanadamu na sayari yetu” ametangaza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, akikutana leo na waandishi wa habari mjini New York. Mara akaeleza ni kwa nini..

“Jana usiku, nchi wanachama waliitikia wito wa kuchukua hatua na kuweka historia kwa kuridhia ajenda kabambe, jasiri na yenye kuleta mabadiliko, ya maendeleo endelevu kwa miaka 15 ijayo.”

Ban amekuwa akizungumza kuhusu hatua ya kuafikia ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015 hapo jana, akiwa ameandamana na Balozi Macharia Kamau wa Kenya na viongozi wengine, waliosimamia mchakato wa mashauriano kuhusu ajenda hiyo.

Ban amesema makubaliano kuhusu ajenda hiyo ni matokeo ya zaidi ya miaka mitatu ya juhudi zilizoanza na kongamano la Rio+20 mwaka 2012, kazi ya jopo la ngazi ya juu la watu mashuhuri, mfumo wa Umoja wa Mataifa, na mchakato wa mashauriano ambao umekuwa jumuishi na wazi zaidi katika historia ya Umoja wa Mataifa.

“Hii kwa hakika na ajenda ya watu. Rasimu ya matokeo ya mashauriano inaitwa: Kubadili ulimwengu: Ajenda yam waka 2030 kwa maendeleo endelevu” na ni barabara ya kutokomeza umaskini, kujenga maisha ya utu kwa wote, kwa kutuomwacha yeyote nyuma. Ni wito pia wa kuongeza juhudi za kuitunza sayari yetu kwa manufaa yetu na vizazi vijavyo.”

Katibu Mkuu amesema ajenda hiyo inakwenda hatua zaidi ya malengo ya maendeleo ya milenia.

“Ina malengo 17 ya maendeleo endelevu, ambayo ni ya pamoja, yanayohusuiana na yasiyoweza kugawanywa. Kwa njia nyingi, malengo haya yanawakilisha ratiba ya mambo ya kufanywa kwa ajili ya watu na sayari dunia. Yanajali watu na sayari. Ni kwa wote, yakilenga nchi zote, huku yakitambua hali na uwezo tofauti.”

Katibu Mkuu amesema malengo hayo yanatoa wito wa kujenga jamii zenye amani, jumishi na zinazotawaliwa vyema, na taasisi zinazowajibika kama msingi wa ufanisi.