Skip to main content

Haki za binadamu zamulikwa DPRK na Jamhuri ya Korea

Haki za binadamu zamulikwa DPRK na Jamhuri ya Korea

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein, ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Korea (Kusini) kwa kukubali kuwa mwenyeji wa ofisi ya haki za binadamu iliyofunguliwa nchini humo, mahsusi kwa ajili ya kufuatilia hali ya haki za binadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea (Kaskazini), DPRK.

Akizungumza na waandishi wa habari mjni Seoul leo, Kamishna Zeid amesema kuwa kufunguliwa kwa ofisi hiyo ni hatua kubwa, na kunaonyesha kuwa kila mmoja ana hamu kubwa ya kutaka kuona hali ya haki za binadamu DPRK ikibadilika kwa kiwango kikubwa, kufuatia ripoti ya tume ya uchunguzi iliyotolewa mnamo Februari 2014.

Amesema watu wa DPRK wamekuwa wakikumbana na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na kunyanyaswa kwa miongo mingi, na sasa ulimwengu umeliweka suala hilo katika ajenda yake, kwani kabla ya ripoti ya tume hiyo ya uchunguzi, ulimwengu ulikuwa ukimulika tu suala la nyuklia pekee.

Kamishna Zeid pia amezungumzia ukame wanaokumbana nao watu wa DPRK wakati huu, akisema kuwa ili kuepusha hatari ya njaa, serikali ya DPRK inapaswa kushirikiana na nchi jirani zake na mashirika ya kibinadamu.

Amesema baadhi ya mambo yatokanayo na DPRK yanaathiri Jamhuri ya Korea Kusini na nchi zingine kama vile Japan, ambako inaaminika kuwa watu 881 wametekwa na kuhamishiwa DPRK.

Aidha, amesema ingawa Jamhuri ya Korea imepiga hatua kubwa kiuchumi na katika kuboresha hali ya haki za binadamu tangu ilipobadilika na kuwa demokrasia miaka 30 iliyopita, bado inakabiliwa na changamoto ambazo nchi zingine zilizoendelea kidemokrasia zinakumbana nazo. Ametoa mfano wa malalamishi ya mashirika ya umma kuhusu kubinywa uhuru wa kujielea na uhuru wa kufanya mikutano ya amani kwa kutumia sheria ya usalama wa kitaifa ya mwaka 1948, ambayo amesema imepitwa na wakati.