Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali Yemen ni mbaya, CERF kuidhinisha dola Milioni 25 kusaidia Yemen

Hali Yemen ni mbaya, CERF kuidhinisha dola Milioni 25 kusaidia Yemen

Mratibu Mkuu wa masuala ya usaidizi wa kibinadamu kwenye Umoja wa Mataifa Stephen O’Brien amerejelea wito unaotaka pande husika kwenye mzozo wa Yemen kuafikiana kusitisha mapigano haraka iwezekanavyo ili kumaliza machungu yanayopata raia wasio na hatia.

Bwana O’Brien amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari kwa njia ya simu kutoka Ujerumani akieleza kuwa huo ndio ujumbe ambao pia walipatia baraza la usalama wakati wa kikao cha faragha kuhusu Yemen siku ya Jumatano.

“Pande katika mzozo zinaonyesha kutojali uhai wa binadamu, kwa kushambulia mara kwa mara maeneo ya raia ikiwemo hospitali, shule, mitambo ya umeme na maji. Mamilioni ya watu wamelazimika kukimbia makwao, na wengine wamelengwa na mashambulio wakati wanakimbia.”

Wakati huo huo kutokana na kuzidi kuzorota kwa haliya usalama Yemen, mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa, CERF unatoa dola Milioni 25 kwa ajili ya kusaidia operesheni za kuokoa maisha ya binadamu  nchini humo.

Bwana O’Brien amenukuliwa na taarifa ya ofisi yake, OCHA akisema kuwa fedha hizo zitasaidia miradi muhimu kama vile kupeleka mafuta, dawa, vifaa vya dharura, maji safi na salama na huduma za kujisafi bila kusahau lishe kwa wahitaji.

Zaidi ya wananchi Milioni 21 wa Yemen ambao ni asilimia 80 ya watu wote wanahitaji msaada ambapo tangu mwaka 2007 Yemen ilipoanza kuhitaji misaada muhimu CERF imeshatoa jumla ya dola Milioni 107 za usaidizi.