Djinnit kuhutubia Baraza kuhusu Burundi kutoka Bujumbura

4 Juni 2015

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo linakuwa na mashauriano ya faragha kuhusu Burundi ambapo mjumbe maalum wa Katibu Mkuu kwenye maziwa makuu, Said Djinnit anatarajiwa kuhutubia kutoka Bujumbura. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Habari zinasema kuwa Bwana Djinnit atahutubia kwa njia ya video kuhusu hali ilivyo nchini Burundi kwa sasa wakati huu ambapo tayari Umoja wa Mataifa kupitia mkuu wake wa masuala ya kisiasa Jeffrey Feltman uliieleza Burundi umuhimu wa kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa na Kikao cha viongozi wa Afrika Mashariki ambaye yameipa serikali ya Burundi fursa mpya ya kuandaa mazingira mazuri kwa ajili ya uchaguzi wenye amani na utakaoaminika.

Halikadhalika kwenye kikao hicho wajumbe watahutubiwa na Adama Dieng, mshauri maalum wa Katibu Mkuu kuhusu uzuiaji wa mauaji ya halaiki, na hotuba yake itajikita katika yale aliyojionea wakati wa ziara yake ya hivi karibuni nchini Burundi.

Umoja wa Mataifa umeendelea kuitaka serikali ya Burundi kuhakikisha kuna amani na utulivu na kuwasihi Warundi kueleza maoni yao kwa njia ya amani huku ikiviomba vyombo vya usalama kujiepusha kutenda ukatili wakati wa kudhibiti maandamano.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter