Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ataka sitisho jingine la kibinadamu kwa mapigano ya Yemen

Ban ataka sitisho jingine la kibinadamu kwa mapigano ya Yemen

Wakati kazi ya maandalizi ya mashauriano ya kisiasa kuhusu Yemen ikiendelea, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amekariri wito wake wa kutaka kuwepo sitisho jingine la kibinadamu kwa mapigano nchini humo, ili kuwezesha ufikishaji wa misaada ya kibinadamu kwa Wayemeni wanaoihitaji.

Hayo ni kwa mujibu wa Msemaji wa Katibu Mkuu, Stephane Dujarric, akikutana na waandishi wa habari leo mjini New York..

“Mahitaji ya kibinadamu yanazidi kuwa makubwa, na hatua za dharura zinapaswa kuchukuliwa na jamii ya kimataifa na mataifa ya kikanda ili kuepusha madhara mabaya zaidi ya mapigano.”

Ofisi ya kuratibu masuala ya kibinadamu, OCHA, imesema kuwa chumba cha operesheni katika Wizara ya Afya katika mji mkuu, Sana’a, ambacho huratibu operesheni zote za kibinadamu, kiliharibiwa hapo jana, na uharibifu huo unatarajiwa kuvuruga zaidi operesheni za huduma za afya, ambazo tayari zinapata shinikizo kubwa. Huyu hapa tena, Bwana Dujarric..

“Tukio la jana linafuatia mashambulizi dhidi ya vituo kadhaa vya afya, tangu mapigano Yemen yalipochacha mnamo Machi 26. Aidha, wahudumu kumi wa afya wameuawa au kujeruhiwa wakati wakifanya kazi zao tangu wakati huo.”

Amesema Shirika la Afya Duniani, WHO linaendelea kutoa wito wa kulinda vituo vya afya, wahudumu na wagonjwa.