Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto waathiriwa hawawezi kusema wala kutafuta haki ya kisheria: UNICEF

Watoto waathiriwa hawawezi kusema wala kutafuta haki ya kisheria: UNICEF

Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa lakuhudumia watoto UNICEF inasema kuwa waathirika wengi wa ukatili hususani watoto huko Ulaya Mashariki na Kati pamoja na Asia ya Kati hawawezi kusema wala kufungua mashtaka mahakamani.

Ikiwa na jina Usawa wa Watoto na Fursa ya Kisheria Ulaya ya Kati na Mashariki pamoja na Asia ya Kati, ripoti hiyo inaangazia vikwazo dhahiri watoto wanavyokabiliana navyo wakati wakitafuta haki na suluhisho mujarabu ili kuweka kando ukosefu wa haki na ubaguzi katika maisha yao.

Hata hivyo inamulika mafanikio katika utawala wa sheria ikisema kuwa serikali katika ukanda huo zinapiga hatua katika michakato ya kimahakama ili kulinda haki za watoto kulingana na viwango vya kimataifa .

Ripoti inasema kuwa msaada wa kisheria na kijamii kwa watoto katika kuwasadia kupata haki zao unatolewa na kasi inaongezeka katika huduma hizo kupitia vituo vya haki za watoto au vituo vya misaada ya kisheria na kupata taarifa kuhusu anuani sahihi za maeneo ya misaada, kupata ushauri wa kisheria na kupelekwa kwa mwanasheria au mshauri wa kisaikolojia.

Pia imesema kuwa wakati mwingine watoto waweza kupata msaada wa kisheria moja kwa moja ilikuanzisha mchakato wa haki.