Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 65 ya mzozo, UNRWA yataka kutafakari hatma ya wakimbizi wa Palestina

Miaka 65 ya mzozo, UNRWA yataka kutafakari hatma ya wakimbizi wa Palestina

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA Pierre Krahenbuhl, amesema ni lazima kutafakari hatma ya wapalestina wakati ambapo UNRWA leo inatimiza miaka 65 tangu kuanzishwa kwake.

Akizungmza na waandishi wa habari Jumatatu mjini New York kabla ya maadhimisho ya miaka 65 ya UNRWA, Pierre Krahenbuhl ameeleza kwamba UNRWA haikutegemea kudumu kwa miaka mingi, lakini ukosefu wa utashi wa kisiasa kwa kutatua mzozo kati ya Israel na Palestine ulilazimisha UNRWA kuendelea na shughuli zake za kibinadamu na za maendeleo.

«  Nadhani  nia  ya kutatua hali hiyo kwa njia ya kisiasa ni msingi wa swala nzima. Si jukumu la UNRWA kuangazia eneo hilo lakini kwa kweli kila siku tunaona gharama ya kibinadamu ya ukosefu wa suluhu ya kisiasa, na tunaona gharama hiyo inapanda. »

Kamishna Krahenbuhl amezingatia mazingira magumu yanayokumba wakimbizi, hasa wale wanaoishi nchini Syria au wakazi  wa Gaza ambao wengi wao bado hawana nyumba baada ya vita vya Julai mwaka jana.

Hatimaye, amepongeza kazi zinazofanywa na UNRWA, akichukua mfano wa jinsi UNRWA iliweza kuwapa hifadhi wakazi  wa Gaza 300,000 wakati wa mzozo na Israel mwezi Julai 2014, akiwashukuru wafanyakazi 25 waliouawa mwaka jana Gaza na Syria.