Skip to main content

Shughuli za kuadhimisha Siku ya Mazingira zaanza

Shughuli za kuadhimisha Siku ya Mazingira zaanza

Shughuli za maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani zimeng’oa nanga hii leo, huku wito ukitolewa kwa serikali, jamii na watu binafsi kuboresha mienendo yao ya matumizi ya rasilmali.

Mwaka huu, kauli mbiu ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo itaadhimishwa mnamo Juni 5, ni ‘Ndoto bilioni saba. Sayari Moja. Tumia kwa kujali.’ Kwa wito huo, watu wanahimizwa kutafakari kuhusu mienendo yao ya maisha na kupunguza athari za vitendo vya wanadamu kwa rasilmali za asili kwa kufanya maaumuzi ya matumizi yenye busara.

Kilele cha maadhimisho ya mwaka huu kitakuwa nchini Italia, ambayo ipo mstari wa mbele katika kuchukua hatua za kimataifa ili kuboresha lishe na matumizi ya rasilmali.

Kwa mujibu wa jopo la kimataifa kuhusu rasilmali la Shirika la Mpango wa Mazingira, UNEP, iwapo mienendo isiyo endelevu ya matumizi na uzalishaji itaendelea, basi ifikapo mwaka 2050, rasilmali za asili zitakazotumiwa kudumisha mienendo hiyo zitakuwa ni sawa na zile za sayari tatu.