Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rasimu ya sheria Kyrgyzstan inalenga kubinya mashirika ya kiraia:

Rasimu ya sheria Kyrgyzstan inalenga kubinya mashirika ya kiraia:

Wakati bunge nchini Kyrgyzstan likijiandaa kujadili rasimu ya sheria kuhusu mamluki, ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imetaka rasimu hiyo iangaliwe upya kwa kuwa jinsi ilivyo itakuwa na madhara kwa shughuli za vikundi vya kiraia vinavyohusika na utetezi wa haki za binadamu.

Msemaji wa ofisi hiyo Rupert Colvillle amesema rasimu hiyo inataka vikundi vya kiraia visivyo vya kibiashara ambavyo vimesajiliwa nchini humo lakini vinajihusisha na masuala ya kisiasa na kupata fedha kutoka nje ya nchi hiyo visajiliwe kama kama mamluki.

Amesema rasimu hiyo hata hivyo imeshindwa kuainisha kwa usahihi neno shughuli za kisiasa badala yake kuelezea kuwa ni shughuli zinazolenga kuchochea mtazamo wa umma kuhusu mchakato huo uliotajwa.

Bwana Colville amesema ainisho hilo linaweka mashakani kazi za mashirika mengi ya kiraia ambayo yanatoa huduma ikiwemo kuchagiza masuala ya haki za binadamu nchini humo.

Halikdhalika linanyanyapaa mashirika hayo na linaweza kujenga chuki na kutokuaminiwa kwa wanaharakati, watetezi wa haki za binadamu na mashirika ya kiraia.