Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Leo ni siku ya kimataifa ya familia, Ban akemea ukatili kwa wanawake na watoto

Leo ni siku ya kimataifa ya familia, Ban akemea ukatili kwa wanawake na watoto

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema ubaguzi dhidi ya wanawake na upuuzwaji wa haki za watoto husababisha ukatili na ukosefu wa fursa za kielimu na afya.

Katika ujumbe wake kwa siku ya kimataifa ya familia yenye ujumbe je wanaume wanawajibika? Ikiangazia umuhimu wa usawa wa kijinsia na haki za binadamu katika familia za sasa, Bwana Ban amesema kote duniani wanawake wanatambulika kama washiriki sawia na wafanyaji maamuzi jambo ambalo amesema linasaidia katika maendeleo yenye usawa kwa watoto.

Hata hivyo amesema ubaguzi dhidi ya haki za wanawake na watoto zinajengwa katika sheria za familia na sera za serikali na hivyo kufanya deturi za kijamii za ubaguzi kukua na kutekelezwa mara kwa mara.

Katibu Mkuu amesema mathalan athari za ubaguzi huo huendelea hadi vizazi vijavyo kwani wengi wa watoto waliopitia ukatili huutekeleza wakikua na kusisitiza kuwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi yenye usawa yanategemea mikakati sawia na kanuni za kijamii zinazounga mkono haki za wanawake na watoto.

Ban katika ujumbe wake amesisitiza kuwa fursa wanazokosa wanawake na watoto kufuatia ukatili zaweza kutatauliwa kwa kubadili kanuni na sheria za kijamii zinazoweza kufuta mfumo dume.