Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makubaliano mapya kuhusu misitu kuchagiza maendeleo endelevu:Sadjik

Makubaliano mapya kuhusu misitu kuchagiza maendeleo endelevu:Sadjik

Makubaliano mapya kuhusu masuala ya misitu ni lazima yalenge kufanikisha maendeleo endelevu na kubadili mwelekeo wa sasa wa ukataji misitu kiholela amesema Rais wa Baraza la kiuchumi na kijamii la Umoja wa Mataifa, ECOSOC Martin Sadjik.

Katika hotuba yake kwenye mkutano wa 11 wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya misitu uliofanyika jijini New York, Marekani Jumatano, Bwana Sadjik amesema makubaliano hayo ni lazima yaibue ushawishi wa uungwaji mkono kisiasa utakaowezesha malengo yake yanatekelezwa.

Amesema anatiwa moyo kuwa mkutano huo unazingatia ujumuishaji wa vipaumbele vya ajenda ya maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015.

Bwana Sadjik amesema azimio thabiti la mawaziri wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa litatoa ujumbe dhahiri juu ya umuhimu wa kuangazia dhima adhimu ya misitu.

Mkutano huo wa wiki mbili utakaomalizika mwishoni mwa wiki hii, unatarajiwa kuibuka na azimio hilo lenye lengo la kuchagiza mwelekeo mpya na thabiti wa rasilimali za misitu duniani