Skip to main content

Pande zote zisitishe vita kunusuru maisha ya watu Yemen: Van Der Klaauw

Pande zote zisitishe vita kunusuru maisha ya watu Yemen: Van Der Klaauw

Mratibu wa Umoja wa mataifa wa masuala ya kibinadamu kwa ajili ya Yemen Johannes Van Der Klaauw amerejea wito wa pande zote kusitisha mapigano na kutoa fursa ya kunusuru maisha ya watu. Flora Nducha na taarifa kamili...

(TAARIFA YA FLORA NDUCHA)

Mratibu huyo amesema anatiwa hofu na taarifa kutoka mjini Aden ambazo zinasema jana Jumatano watu kadhaa wameuawa wengi wakiwa ni raia wakiwemo wanawake na watoto, na kuwaacha wengine wangi wakijeruhiwa katika mapigano.

Raia wamearifiwa kulengwa wakati wakijaribu kukimbia kwenda kwenye maeneo salama baada ya kukwama Aden wakikikosa huduma muhimu kama maji, chakula na huduma za afya kwa wiki kadhaa sasa.

Hivyo amerejea wito wake kwa pande zote kuheshimu usitishaji mapigano ili kuruhusu watu hao kuondoka na kupata huduma muhimu, akisistiza kuwa kuwalenga raia , wafanyakazi wa misaada, na mashambulizi dhidi ya hospital na miundombinu mingine ya raia ni lazima vikome mara moja. Trond Jensen ni mkuu wa OCHA Yemen anasema hali inaelekea kuwa janga kubwa.

(SAUTI YA TROND JENSEN)

"Tunashuhudia uwezekano wa janga kubwa, kile tunachokiona ni taasisi nyingi kufungwa, kwa sababu ya kukosekana kwa mafuta, hizi ni Hospitali  ambazo zina upungufu wa kasi wa mafuta ya kuendesha jenereta zao, tunaona masoko yakifungwa ambayo yanasabisha upatikanaji wa chakula kupungua sana, na Hiyo inaleta wasiwasi mkubwa".