Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vanuatu hatarini kukumbwa na njaa

Vanuatu hatarini kukumbwa na njaa

Wiki mbili baada ya kimbunga PAM kushambulia visiwa vya Vanuatu, Mratibu wa Misaada ya kidinadamu nchini humo, Osnat Lubrani, ametembelea jimbo la Tafea ambalo ni miongoni mwa visiwa vilivyoathirika zaidi.

Bi Lubrani amesema, licha ya jitihada za serikali za kufikisha maji, vyakula na huduma za afya katika kila kisiwa, bado hali ya dharura haijaisha na ni lazima kuongeza bidii ili kuzuia hatari ya njaa nchini humo. Akieleza kwamba asilimia 90 ya mazao yameharibiwa na kimbunga, huku wengi wa raia wa Vanuatu wakiwa ni wakulima, amesema ni muhimu kupeleka misaada ili kupambana na hatari ya ukosefu wa usalama wa chakula.

Hata hivyo amepongeza raia wa Vanuatu kwa ujasiri wao, wakiwa tayari wameanza kujenga upya maisha yao kupitia misaada ya serikali na jamii ya kimataifa.

Tayari mashirika ya Umoja wa Mataifa na yale yasiyo ya kiserikali yamewapatia wakulima wa Vanuatu mbegu ili kuhakikisha usalama wa chakula kwa muda mrefu, na yameshirikiana na serikali ili kujenga upya miundombinu na kurejesha shughuli za uchumi.

Bado zaidi ya dola millioni 20 zinahitajika ili kuwasiadia raia wa Vanuatu 166,000 kwa kipindi cha miezi mitatu.