Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huduma ya maji yasalia anasa kwa baadhi ya wakazi duniani

Huduma ya maji yasalia anasa kwa baadhi ya wakazi duniani

Wakati suala la kupata maji safi na salama limeripotiwa kuwa moja ya mafanikio ya malengo ya maendeleo ya milenia, bado watu Milioni 748 duniani kote wanakumbwa na mkwamo kwenye kupata huduma hiyo adhimu.

Hiyo ni kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF katika taarifa yake iliyotolewa Ijumaa kuelekea siku ya maji duniani tarehe 22 mwezi huu.

Sanjay Wijesekera Mkuu wa programu ya UNICEF duniani inayohusika na maji ametaja mataifa ambayo huduma ya maji safi na salama imesalia kuwa anasa zaidi kuwa ni Msumbiji, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na Papua New Guinea.

Amesema kwa watoto ukosefu wa maji ni janga kwa ni karibu watoto Elfu Moja hufariki dunia kila siku kutokana na magonjwa ya kuhara yanayohusiana na ukosefu wa maji safi na salama na huduma za kujisafi.

Halikadhalika kwa wasichana na wanawake, harakati za kusaka maji zinawapunguzia muda wa kuwa na familia zao, kusoma na pia kuhatarisha kukumbwa na visa vya ukatili wa kingono.

UNICEF imesema nchi nyingi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara haziko katika mwelekeo wa kufikia kiwango cha kupunguza kwa asilimia 50 watu wasio na huduma hiyo ya maji safi na salama.

Shirika hilo limekumbusha kuwa huduma ya maji safi na salama ni haki ya msingi ya binadamu.