Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Stephen O’Brien ndiye anamrithi Valerie Amos OCHA

Stephen O’Brien ndiye anamrithi Valerie Amos OCHA

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon leo ametangaza uteuzi wa Stephen O’Brien wa Uingereza kama msaidizi wa Katibu Mkuu kwa masuala ya kibinadamu katika ofisi ya kuratibu masauala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA.

O’Brien anachukua nafasi ya Valerie Amos ambaye pia anatoka Uingereza na ambaye Katibu Mkuu anamshukuru sana kwa huduma bora aliyoitoa kwa Umoja wa mataifa na jumuiya ya masuala ya kibinadamu , kwa kufanya kazi bila kuchoka kusaidia watu waliohitaji msaada duniani.

Bwana O’Brien ana uzoefu mkubwa anaokuja nao Umoja wa Mataifa katika masuala ya diplomasia ya kimataifa na utetezi, pamoja na usimamizi katika uratibu wa jitihada za masuala ya kibinadamu, hasa katika mapambano ya dhidi ya malaria na magonjwa ya kitripiki yaliyosahaulika. Pia mchango wake mkubwa kwa kuchagiza taifa lake kufikia lengo la utoaji misaada ya maendeleo kwa asilimia 0.7%ya jumla ya pato la taifa.

Hivi sasa Bwana O’Brien ni mbunge wa jimbo la Eddisbury nchini Uingereza na ni mwakilishi maalumu wa waziri mkuu na serikali ya Uingereza kwa Sahel tangu mwaka 2012. Anashirikiana na kufanya kazi pamoja na wadau wengine wa kimataifa kutafuta Amani ya kudumu Mali na mataifa jirani .

Bwa O’brien amewahi kushika nyadhifa mbalimbali zikiwemo naibu waziri wa maendeleo ya kimataifa kuanzia 2010-2012, waziri kivuli wa afya na huduma za jamii 2005 hadi 2010 na pia nyandhifa nyingi za kujitolea kama mwanzilishi na mwenyekiti wa kundi la wabunge la kukabiliana na malaria na magonjwa yaliyosahaulika tangu mwaka 2004.

Bwana O’brien alizaliwa nchini Tanzania , ana stashahada ya udhamili katika masuala ya sheria kutoka chuo kikuu cha Cambridge. Ameoa na ana watoto watatu.