Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wanaoingizwa jeshini na pande zote waachiliwe Sudan Kusini: Zerrougui:

Watoto wanaoingizwa jeshini na pande zote waachiliwe Sudan Kusini: Zerrougui:

Utoaji wa mafunzo na kuwaingiza watoto jeshini ni changamoto kubwa inayoendelea Sudan Kusini licha ya hakikisho la serikali na upinzani unaoongozwa na Riek Machar kuwalinda watoto kutokana na athari za vita, amesema Bi Leila Zerrougui mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu kwa watoto walio katika vita vya silaha.

Bi Zerrougui amesema hakuna watoto walioachiliwa na kundi la SPLA (Sudan People’s Liberation Army) au upande wa upinzani wa Riek Machar, badala yake taarifa zinazopokelewa zinasema mamia ya watoto wapya wamechukuliwa kama wanajeshi na makundi ya wanamgambo yanayohusiana na serikali au upinzani wa SPLA.

Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa umekusanya ushahidi kwamba wanamgambo wanaongozwa na kamanda Johnson Oloni, wa SPLA ndio wanaohusika na utekaji wa takriban watoto 89 na pengine mamia ya watoto wa eneo la Wau Shilluk katikati ya mwezi wa Februari.

Amesema hakutakuwa na Amani ya kudumu Sudan Kusini endapo watoto watabaguliwa na ndio sehemu kubwa ya raia wa taifa hilo. Amesema watoto hao ni lazima waachiliwe na kuna haja ya kuwajibika kwa wale wanaotoa mafunzo na kuwaingiza watoto jeshini, kwa kukiuka haki za watoto.