Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanaokimbia mizozo wasitumbukie mtego wa wasafirishaji haramu: UNODC

Wanaokimbia mizozo wasitumbukie mtego wa wasafirishaji haramu: UNODC

Mkutano wa kimataifa kuhusu usafirishaji  holela wa wahamiaji kwa njia ya bahari umefanyika jijini London, Uingereza ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayopambana na madawa ya kulevya na uhalifu, UNODC Yury Fedotov amesema hatua za dharura zinahitajika ili kudhibiti vikundi vya uhalifu vinavyonyemelea wahamiaji.

Amesema boti zilizobeba abiria kupindukia, kutelekezwa kwa meli za mizigo na hata wahamiaji kutelekezwa baharini bila kufahamu la kufanya ni moja ya majanga makuwba duniani.

Bwana Fedotov amesema haikubaliki kabisa kuwaacha watu wanaokimbia majanga kwenye nchi zao kutumbukia kwenye mtego wa vikundi vya uhalifu na hivyo lazima hatua za dharura zichukuliwe kuokoa maisha  yao.

Amesema UNODC kwa upande wake tayari imeandaa mkakati mpya utakaosaidia jitihada za kimataifa za kuokoa wahamiaji kwenye bahari ya Mediterranean.

Msingi wa mkakati huo ni utafiti na upembuzi, kuimarisha uwezo wa nchi kuandaa mifumo thabiti ya kudhibiti uhalifu, kuendelea ushirikiano na kujenga uratibu na ulinzi wa haki za wahamiaji.

Mkutano huo wa London, umeandaliwa kwa pamoja na mashirika mbali mbali ikiwemo lile la masuala ya baharini, IMO na lile la wakimbizi, UNHCR