Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asilimia 75 ya watu duniani hawapati dawa za kupunguza maumivu- ripoti

Asilimia 75 ya watu duniani hawapati dawa za kupunguza maumivu- ripoti

Takriban watu bilioni 5.5 bado hawana uwezo wa kupata dawa zinazopunguza maumivu, imesema ripoti mpya ya Bodi ya Kudhibiti Dawa Duniani, INCB, ambayo imezinduliwa leo mjini London. Anayetupasha zaidi, ni Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Ripoti hiyo ya INCB imesema kuwa asilimia 92 ya dawa zenye codeine au morphine – ambayo hutengenezwa kutoka zao la afyuni - hutumiwa na asilimia 17 tu ya idadi ya watu kote duniani, ambao wanaishi hususan katika nchi za Marekani, Canada, Ulaya Magharibi, Australia na New Zealand, huku upatikanaji wa dawa hizo ukiwa haba, au haupo kabisa kwa asilimia 75 ya watu duniani.

Ripoti ya INCB pia imesema kuwa tatizo la matumizi ya dawa za kulevya au utumiaji mbaya wa dawa za kupunguza mamumivu pia linaongezeka.

Dkt. Lochan Naidoo ni rais wa INCB, na anaeleza kinachopawa kufanyika ili kukabiliana na hali hii.

(Sauti ya Naidoo)

“Mwaka huu tunaangazia kuzihimiza serikali kuchukua mwelekeo wenye uwiano kuhusu tatizo la dawa duniani. Sekta ya dawa na sisi tulio kwenye nafasi hii, tunapaswa kuweza kuzihimiza serikali zimakinike zaidi kutokana na kuongezeka kwa matumizi mabaya ya dawa kote duniani.”

Ripoti hiyo imependekeza kuwa ili kufikia njia inayokabiliana na suala la dawa, serikali zinapaswa kuhakikisha kuwa kupunguza kwa mahitaji ya dawa hizo ni moja ya mambo ya kipaumbele katika sera za kudhibiti matumizi ya madawa ya kulevya kama vile heroini inayotokana pia na zao la afyuni, huku zikijikita zaidi katika kusaidia na kuwekeza rasilmali katika kuzuia, kutibu na kurekebisha watu wenye uraibu wa matumizi ya dawa za kulevya.

Bodi hiyo imezitaka nchi zitimize wajibu wao chini ya mikataba ya haki za binadamu, na pia zipige marufuku adhabu ya kifo pale zinapofanya uamuzi kuhusu makosa yanayohusiana na dawa za kulevya.