G20 itimize ahadi zake za kukuza uchumi: IMF

11 Februari 2015

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la fedha duniani, IMF Christine Lagarde, amezitaka nchi za G20 kutimiza wajibu wao wa kisera kwa mujibu wa tamko la Brisbane la kuinua ukuaji wa uchumi wa nchi hizo.

Akizungumza mjini Istanbul kwenye mkutano wa mawaziri wa fedha wa G20, Lagarde amesema hatua hiyo inaweza kuinua ukuaji wa nchi hizo kwa asilimia Mbili na hatimaye kutengeneza fursa mpya milioni za ajira katika kipindi cha miaka minne ijayo.

Amesema mwaka huu ni fursa pekee duniani akipongeza Uturuki ambayo ni rais wa sasa wa G20 kwa kujumuisha ajenga ya maendeleo baada ya mwaka 2015 katika vipaumbele vya mipango ya kundi hilo.

Mkuu huyo wa IMF ametaja mambo matatu yanayoweza kujenga malengo endelevu thabiti kwa karne ya 21 kuwa ni mkutano wa uchangishaji fedha kwa maendeleo, utekelezaji wa malengo endelevu na mkutano wa kilele wa mabadiliko ya tabianchi.

Amesema jamii ya kimataifa ni lazima ishirikiane kwa dhati na kutumia fursa hiyo ipasavyo na IMF itatekeleza majukumu yake kwenye maeneo hayo.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter