Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNSMIL yalaani vikali kuanza tena mashambulizi eneo la mafuta Libya

UNSMIL yalaani vikali kuanza tena mashambulizi eneo la mafuta Libya

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, UNSMIL, limelaani vikali shambulizi lililofanywa na makundi yenye silaha yaliyoko chini ya Operesheni ya Alshuruq katika eneo la Oil Crescent nchini Libya, mnamo tarehe 3 Februari 2015, na ambalo liliwaua watu wengi.

Katika taarifa, UNSMIL imesema shambulio hilo limeonyesha kuvunjwa kwa ahadi zilizowekwa na makamanda wakuu kwamba wangejiepusha na vitendo vinavyoweza kuvuruga mchakato wa kisiasa wakati wadau Libya wakifanya bidii kujenga daraja ya ushirikiano ambao utachangia utatuzi wa mzozo wa Libya kwa njia ya amani.

UNSMIL imesema shambulizi hilo pia linadhoofisha juhudi za kufikia suluhu la kisiasa na kuhatarisha rasilamali ya mafuta, ambayo ni mali ya watu wa Libya.

UNSMIL imekumbusha makundi yote yenye silaha kwamba watu kwa wingi zaidi nchini Libya wanataka amani na utulivu urejeshwe nchini mwao, na hivyo kuyatolea wito yatimize ahadi za awali za kusitisha mapigano na vikosi vyao kuweka chini silaha ili kuunga mkono mchakato wa kisiasa.