Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Upungufu wa fedha waathiri familia za wakimbizi wa ndani Gaza

Upungufu wa fedha waathiri familia za wakimbizi wa ndani Gaza

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwasaidia Wakimbizi wa Palestina, UNRWA, bado linahitaji dola milioni 500 ili kusaidia watu ambao walipoteza nyumba zao wakati wa mapigano ya mwezi Julai, mwaka uliopita.

Kwa mujibu wa msemaji wa UNRWA, Chris Gunness, ambaye ameongea na waandishi wa habari kutoka Palestina, hali ni tete kwani baadhi ya miradi iliyokuwa inasaidia familia za Gaza imesimamisha kwa sababu ya upungufu wa ufadhili.

“Hali kwa familia ambazo zinategemea msaada huu ili kujenga nyumba zao upya itakuwa mbaya sana, bila shaka. Kuna aina mbili za watu. Kuna wale ambao wamepata pesa kidogo na wameanza kujenga upya nyumba zao, na hawatapata kitu chochote, msaada umesitishwa. Kuna wale ambao hawajawahi kupewa msaada, wameambiwa kwamba hawatapata kitu kwa sasa hivi. Juu ya hiyo baadhi ya pesa hizo zilikuwa kwa ajili ya kusaidia watu kulipa kodi zao. Kwa hiyo watu hawa ambao walikuwa wanategemea msaada huo kulipa kodi, hawataweza kulipa kodi zao, wanaweza kubaki bila makazi.”

Hata hivyo, ameongeza kwamba Saudi Arabia imetoa mchango wa dola milioni 55 kwa ajili ya ukarabati wa Gaza.