Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Honduras itumie uzoefu wake kwenye ajenda baada ya 2015:Ban

Honduras itumie uzoefu wake kwenye ajenda baada ya 2015:Ban

Mwaka huu ni wa kuchukua uamuzi sahihi kuhusu maendeleo endelevu na Honduras ina nafasi muhimu kwa kuzingatia ni mwanachama mpya wa Baraza la masuala ya kijamii na kiuchumi la Umoja wa Mataifa, amesema Katibu Mkuu Ban Ki-Moon alipozungumza na waandishi wa habari mjini Tegucigalpa, Honduras aliko ziarani.Ban amesema dhima hiyo ya Honduras inatiwa chachu zaidi na uzoefu kwenye mpango wake wa maisha bora kwa wote kwani umejikita katika masuala ya amani, fursa za ajira zenye hadhi na hifadhi ya jamii.

Amepongeza kuimarika kwa usalama nchini Honduras akitolea mfano kupungua kwa kiwango cha mauaji kutoka watu 86 kati ya watu Laki moja hadi watu 66 kwenye kiwango hicho.

Hata hivyo ameeleza wasiwasi wake juu ya hatma ya watoto wahamiaji kutoka Amerika ya Kati wanaokimbia nchi zao wakiwa peke yao akitaka hali yao ishughulikiwe halikadhalika utu na haki za binadamu zizingatiwe.

Amesema Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia jitihada za kikanda za kushguhulikia masuala ya usalama ikiwemo kubadilishana uzoefu wa jinsi ya kudhibiti uhalifu, ghasia miongoni mwa vijana na kujumuisha katika jamii watu walioachana na uhalifu.