Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wabunge tungeni sera zenye maslahi kwa wananchi: Ban

Wabunge tungeni sera zenye maslahi kwa wananchi: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon anaendelea na ziara yake nchini Honduras ambapo leo atazuru eneo la urithi wa dunia huko Copan Ruinas. Taarifa kamili na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Ban atatembelea eneo hilo kabla ya kuelekea nchini El Salvador wakati huu akiwa ameshazungumza na viongozi mbali mbali Honduras ikiwemo kuhutubia Bunge la nchi hiyo kwenye mji mkuu Tegucigalpa.

Katibu Mkuu amewaeleza wawakilishi hao wa wananchi kuwa mustakhbali wa taifa hilo uko mikononi mwao kwani wanabeba matumaini ya wananchi.

Ametaka wakumbuke kuwa wao ni wabunge na hivyo wana jukumu la kugeuza matarajio ya wananchi kuwa sera zinazoweza kuleta mabadiliko kwa manufaa ya wananchi wote.

Ban amesema viongozi hao ni lazima wakumbuke wanawajibika kwa wananchi na licha ya kwamba Honduras imeibuka kutoka vuguvugu la kisiasa hivi karibuni bado kuna changamoto za kushughulikia.

Mathalani amesema theluthi mbili ya wananchi bado ni mafukara, huku theluthi moja tu ya vijana wanamaliza masomo ya sekondari ya juu na fursa za ajira zenye hadhi zikisalia kuwa ni chache.

Katibu Mkuu amekumbusha kuwa umaskini na ukosefu wa usalama vinakwenda pamoja kwa hivyo ni vyema Honduras kuchukua hatua siyo tu kuimarisha usalama wa ndani bali pia kushirikiana kikanda ili kuimarisha usalama wake.