Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu kwanza Sudani Kusini,mengine yatafuatia: UNMISS

Elimu kwanza Sudani Kusini,mengine yatafuatia: UNMISS

Kaimu mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, Toby Lanzer amesema ukosefu wa amani na utulivu umesababisha maelfu ya watoto kukosa haki ya elimu nchini humo na sasa kipaumbele kinaelekezwa katika kampeni ya kuwarejesha shuleni mwaka huu.

Katika mahojiano na radio ya Umoja wa Mataifa Lanzer amesema licha ya kwamba misaada ya kibinadamu hususan chakula inahitajika mwanzoni mwa mwaka, bado elimu inapaswa kupewa umuhimu mkubwa kwa mustakabali mwema wa taifa la Sudani Kusini

(SAUTI LANZER)

"Kuhakikisha kuwa wanapata fursa ya kurejea shuleni, tunachojaribu kufanya kwa kushirikiana na wizara ya elimu, na mashirika ya kimataifa kama vile UNICEF, na asasi za kiraia, ni kuwasaidia watoto nusu milioni kurejea katika shule zenye vitendea kazi na walimu wenye shauku ya kuona watoto wanaendelea."

Hata hivyo Lanzer amesema changamoto kubwa kwa sasa inayokabili Sudani Kusini ni makubaliano endelevu ya amani.